Kwa nini tuna mwazimisha mwanaume wa Kitanzania

Mabadiliko na changamoto zitokanazo na usasa na utandawazi, zinaendelea kuikumba jamii ya kitanzania. Mwanaume wa kitanzania mwenye kuthamini na kuziishi mila na desturi za kitanzania ni zao la malezi bora. Wahenga walisema “kuzaa si kazi, kazi ni kulea” wakimaanisha kuwa kulea ni kazi zaidi kuliko kuzaa. Pamoja na faida mbalimbali za utandawazi kama ukuaji na maboresho ya teknolojia za mawasiliano na akili bandia, kumekuwepo na ongezeko la ugumu katika malezi ya vijana na watoto. Hivyo, jukumu la kuwapata wanaume wa kitanzania siyo rahisi tena. Jukumu la malezi siyo tena la jamii nzima kama ilivyokuwa zamani katika jamii za kitanzania. Hapo awali, wazazi walikaa na watoto muda mwingi waki wafunda. Wazazi wa kike walikaa muda mwingi na watoto wa kike wakiwafundisha majukumu mbalimbali ya wanawake. Vivyo hivyo, wanaume walikaa muda mwingi na watoto wa kiume wakiwafundisha maswala mbalimbali. Baada ya hapo, kulikuwepo na mafunzo maalumu kutoka kwa wabobezi yaliyo fahamika kama jando na unyago ambako wanajamii wali wafunda wanawake na wanaume ili kuwaandaa na majukumu ya kijamii. Mila hizo zilipelekea uwepo wa jamii za kitanzania zenye kuheshimu utu, zenye mshikamano, zenye upendo baina ya wanawake na wanaume, na zenye utayari wa kulinda jamii. Pamoja na changamoto za usasa na utandawazi, ni ndoto yetu kuona jamii zetu zinarejesha upendo, umoja, amani, na mshikamano kulingana na mila na desturi za kitanzania. Hii ikiwa ni pamoja na kutumia maendeleo katika teknolojia kudumisha tunu za taifa letu na siyo kinyume chake.
Kurejesha jamii ya kitanzania inayojivunia utanzania wetu si kazi rahisi kutokana na mabadiliko yatokanao na utandawazi. Kiwanda tunacho kitegemea katika kumzalisha mwanaume wa kitanzania ni familia yenye upendo ambapo baba na mama wamewezeshwa kuitunza familia yao. Hapa tuna hitajika kuziwezesha familia zinazoweza kutumia fursa zitokanazo na utandawazi na kuzi epuka athari zitokanazo na mitandao katika kulea watoto. Familia imara zitajenga taifa imara ambapo wanaume na wanawake wanashirikiana kama ilivyo kuwa awali. Na hapo ndio tutakuwa na uhakika wa kuifanya Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani.
Ni changamoto zipi anazo kumbana nazo mwanaume wa kitanzania

Kuna changamoto nyingi: katika ngazi ya familia, jukumu la malezi limeongezeka kwa baba na mama ambao nao wamekumbwa na changamoto nyingi zitokanazo na utandawazi na usasa. Wazazi wa jinsi zote wamejikuta wakitumia muda mwingi katika shughuli za kupata kipato kwa ajili ya familia. Majukumu hayo yamepelekea kutokuwepo nyumbani kwa muda mwingi. Katika muktadha huo, jukumu la malezi linafanywa na wadada wa kazi au ndugu ambao wana uzoefu mdogo katika malezi. Kuna madhara yameripotiwa sehemu mbalimbali za taifa ambapo Watoto wameathirika. Kwa mantiki hiyo, tuna janga la kitaifa katika kumzalisha mwanamme wa kitanzania na mwanamke wa kitanzania anaye thamini mila na desturi za kitanzania.
Wakati juhudi za kumjengea uwezo mwanamke (ambazo kwa kiasi kikubwa hazikutoa kipaumbele katika kumjenga mwanamke wa kitanzania anaye thamini mila, destruri, na nafasi yake kama mwanamke wa kitanzania) zinaonyesha mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupatikana fursa za kuajiliwa na kujiajiri na hivyo kulazimika kuwa mbali na nyumbani, wanaume wa Kitanzania, kwa kiasi fulani, imechukuliwa hawahitaji kujengewa uwezo ili waweze kujitegemee. Kitendo hicho, kimepelekea wanaume hao kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yao kama wanaume. Kuna wanaume ambao wameaanza kujihusisha na madawa ya kulevya, kuwa tegemezi kwa wanawake wenye kipato maarufu kama “mashangazi” na wao kugeuka kuwa “vibetini”, kupoteza muda mwingi kwa kushinda vijiweni wakipiga zogo, nakuji husisha na mambo mengine maovu kinyume na maadili ya kitanzania.
Lakini pia mwanaume wengi wa Kitanzania wa sasa hawana rasilimali kama alivyokuwa awali na hivyo kupelekea kukwepa majukumu katika familia na jamii kama ilivyo kuwa zamani. Kwa mfano siku za awali, wanaume wengi wa kitanzania walioa baada ya kufikia umri fulani na baada ya kupata mafunzo kuhusu taasisi ya familia. Lakini kijana wa kiume wa kitanzania wa sasa, tofauti na ilivyo kwa wanawake wanopewa mafunzo walau kupitia”sherehe ya Jikoni” (kitchen party) hapati mafunzo zaidi ya yale yanayotolewa katika baadhi ya taasisi za dini. Wengi hujifunza kupitia mitandao ya kijamii ambayo hutoa elimu kinyume na maadili ya kitanzania. Hivyo, kwa baadhi ya wanaume wanoingia katika ndoa hushindwa kutunza familia zao na hivyo kuzikimbia familia hizo. Viyo hivyo, vijana wengi wanakwepa kuoa kwa kuogopa majukumu yatokanayo na ndoa. Mazingira hayo, yanapelekea ongezeko la mahusiano nje ya ndoa na kupelekea familia zenye Watoto wanaolelewa na mama pekee na watoto wa mitaani. Pia imekuwa ni jambo la kawaida kwa wanaume wa leo kukataa ujauzito, tofauti na siku za nzuma. Ikumbukwe kihistoria, jamii za kitanzania zilikuwa na wanaume na wanawake wawajibikaji; hazikuwa na watoto wa mitaani kwani watoto walilelewa na jamii baada ya wazazi wao wote kutangulia mbele za haki. Hayo ni baadhi ya mambo yanayo likumba taifa letu.
Historia ya siku ya mwanaume wa Kitanzania
Chimbuko la wazo
Maadhimisho ya Siku ya Mwanaume wa Kitanzania yalikuwa ni matokeo ya jitihada za kuonyesha umuhimu na mchango wa wanaume katika jamii, hatua iliyochukuliwa na Asasi ya maendeleo ya jamii (CDA) kwa ushirikiano na Shirika lisilo la Kiserikali la AGEN. Historia ya maadhimisho haya inaanzia na maoni yaliyotolewa na wanachama wa JUKWAA LA MIJADARA HURU TZ, ambalo ni jukwaa la WhatsApp linalokusanya watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania. Jukwaa Hilo lina wanachama Zaidi ya 700. JUKWAA LA MIJADARA HURU TZ lilianzishwa mnamo tarehe 11/11/2017 na Dkt. R. Madaha likiwa na lengo la kuchochea mijadara huru isiyofungamana na imani au itikadi yoyote.
Tamaa ya kutaka kuwa na siku maalumu ya kumkumbuka na kumshukuru mwanaume wa Kitanzania ilizaliwa baada ya kuona umuhimu wa kuthamini mchango wa wanaume katika jamii, hasa ikizingatiwa kuwa mjadala wa usawa wa kijinsia mara nyingi huwa unazingatia zaidi wanawake. Wadau wa maazimisho ya mwanamme wa kitanzania waliona haja ya kuanzisha siku hii kwa lengo la kuleta mwangaza kuhusu mchango wa mwanaume katika jamii na kuhakikisha kuwa anapata haki sawa na heshima inayostahili.
Utekelezaji

Maazimisho ya siku ya mwanaume wa kitanzania yalifanyika kwa mara ya kwanza siku ya Jumanne, tarehe 23 Aprili 2024. Maazimisho hayo yalibeba nguvu ya asili na msisimko wa kipekee na yaliwavutia watu kutoka pande zote. Ingawa anga lilikuwa lina mvua ya dhati, hamasa na shauku ya washiriki haikupungua, bali ilizidi kuwaka, ikionyesha azma yao ya dhati katika kuadhimisha na kuenzi mchango wa wanaume wa kitanzania katika jamii na taifa kwa ujumla.
Pamoja na matone ya mvua yanayong’ara kwenye ardhi, maandamano ya amani yalifungua pazia la matukio ya kuvutia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwanaume wa Kitanzania. Washiriki walionekana kujawa na shauku, wakizungukwa na hisia za uzalendo na umuhimu wa kuenzi mchango wa mwanaume katika jamii. Kama mwamba usioyumbishwa na dhoruba, walipiga hatua za thabiti mbele, wakionyesha azma yao ya dhati katika kuhakikisha kuwa sauti ya mwanaume inasikika na kuthaminiwa.
Katika umbali wa kilomita kadhaa, maandamano haya ya kipekee yalizunguka eneo la Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na mitaa mbalimbali ya mjini Morogoro, yakichota hisia za hamasa kutoka kwa washiriki waliokuwa wakijiunga na kundi hilo kwa shauku na furaha.
Ngoma za moyo na nyimbo za matumaini zilijazana mitaani, zikichagiza moyo wa umoja na mshikamano kati ya washiriki wa maandamano. Hakuna kizuizi kilichoweza kuzuia ujumbe wa umuhimu wa Siku ya Mwanaume wa Kitanzania wa mwaka 2024 “MWANAUME WA KITANZANIA, UZALENDO NA UWAJIBIKAJI” kusambaa kote kwenye kila kona ya mji. Kwa kila hatua, waliohojiwa walisimulia hisia zao kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango wa mwanaume katika jamii.
Maandamano haya hayakuleta tu msisimko wa kipekee, bali pia yalichochea mjadala mpana kuhusu wajibu wa mwanaume katika jamii ya leo. Kwa kila mkondo wa barabara, jumbe zilizoandikwa kwa mikono zilisisitiza umuhimu wa kumkumbuka na kumthamini mwanaume katika kujenga jamii yenye mafanikio. Na hivyo, maandamano haya yalikuwa kama taa ya mwongozo, yakionyesha njia ya kuunganisha na kujenga mustakabali bora kwa kizazi kijacho.
Mazungumzo na Mada Kuu (Kujenga Fikra Mpya na Mchango wa Mwanaume)
Katika uwanja wa mazungumzo na mijadala, Maadhimisho ya Siku ya Mwanaume wa Kitanzania yalikuwa ni fursa ya kipekee ya kujenga fikra mpya na kuzungumzia mchango muhimu wa mwanaume katika jamii. Kwa muda wa kipekee, watu walijikusanya pamoja kujadili masuala muhimu yanayohusu wanaume na jamii kwa ujumla.
Ushuhuda wa Viongozi
Mgeni rasmi, mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Morogoro, Afisa tarafa Ndg. Wilfred Kipako, alitumia jukwaa hilo kutoa wito wa kutambua mchango wa mwanaume katika kujenga taifa na kuimarisha familia. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili wanaume na kusisitiza umuhimu wa siku hiyo katika kukuza uelewa wa umuhimu wa mwanaume katika jamii.
Wito wa Uwajibikaji
Dr. Rasel Madaha, ambaye ni mhadhiri mwandamizi (kwa sasa ni Profesa Mshiriki), mkurugenzi wa AGEN na mlezi wa CDA, alitoa wito wa kufanya kazi kwa pamoja katika kuthamini mchango wa mwanaume katika jamii. Alisisitiza umuhimu wa kuunda mazingira yanayowawezesha wanaume kushiriki kikamilifu katika malezi na ujenzi wa jamii.
Nafasi ya Viongozi Vijana
Mwenyekiti wa CDA, Ndege Mgoma, alielezea umuhimu wa siku hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa maadhimisho hayo yanakuwa endelevu. Alihimiza vijana kushiriki kikamilifu katika kuendeleza mjadala kuhusu mchango wa mwanaume katika jamii na kujenga mustakabali bora kwa kizazi kijacho.
Kwa hakika, mazungumzo haya yalikuwa ni fursa ya kipekee ya kusikiliza sauti za viongozi na kupata mwongozo katika kuelewa na kutathmini mchango wa mwanaume katika jamii.
Hitimisho
Sasa, ni ukweli usiofichika kuwa mwanaume wa kitanzania anatakiwa achukue nafasi yake kuilinda jamii ya kitanzania. Ndoto yetu ni kumwamsha mwanaume wa kitanzania ili awajibike kwa familia na jamii, ili asambaze upendo kwa familia, jamii, na taifa kwa ujumla; ili uchukue jukumu lake kuitunza familia ikiwa ni pamoja na watoto, wake zao, na wanawake wengine. Pia ikitokea amesababisha uja uzito nje ya ndoa awajibike kumtunza mtoto huyo, na siyo kukwepa jukumu hilo. Tuna ndoto ya kuona Tanzania ambapo watanzania wanapendana, ndoa zinadumu, wanaume wanawajibika, na hakuna watoto wa mitaani. Taifa halitaweza kuendelea endapo mwanamme ataachwa nyuma. Wahenga walisema, kila nyuma ya mafanikio ya mwanaume kuna mwanamke; sisi tuna ongezeka kuwa kila nyuma ya mafanikio ya mwanamke kuna mwanaume. Tuna thubutu kusema: “mwanume wa kitanzania mkombozi wa jamii na chachu ya mabadiliko”.